Saturday, May 20, 2006

Haki za wanyama Tanzania

USAFIRISHAJI WA NG’OMBE

Tanzania imejaliwa kuwa na viumbe hai wengi, wakiwemo Binadamu na N’gombe.
Ng’ombe ni mifugo inayofugwa katika kila sehemu ya nchi yetu, kwani ni pato lianlotegemewa kuendeshea maisha ya watu wengi vijijini na mijini.

Kutokana na Ng’ombe kuwa ni pato linalotegemewa na wengi, hivvo kumekuwa na biashara kubwa ya Ng’ombe katika kila pembe ya nchi yetu hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na sehemu nyingine.

Jiji la Dar es salaam linakadiriwa kupokea Ng’ombe zaidi ya 100 kwa siku kutoka katika mikoa ya Shinyanga, Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya na sehemu nyingine. Ng’ombe hao husafirishwa kwa njia ya Barabara na Reli, yaani, kwa kutumia magari na mabehewa.

Safari ya kusafirisha Ng’ombe kuelekea Dar es Salaam inachukua siku kadhaa kutegemeana na umbali wanakotoka. Kwa mfano, Ng’ombe kutoka Shinyanga kwa njia ya Treni inachukua kati ya siku 5-7 mpaka kufika kwenye mnada wa pugu.

Kawaida kisheria katika kusafirisha wanyama kwa njia Treni kuna mabehewa maalumu ya kubebea wanyama kama Ng’ombe ambayo yanakuwa na paa la kuzuia mvua na jua, na madirisha makubwa kwa ajili ya kupitisha hewa, pia Ng’ombe wanatakiwa kuhudumiwa chakula na maji katika safari yao.

“Lakini ikumbukwe kuwa wanyama wanahisi maumivu kama ilivyo kwa Binadamu”.

Kitendo cha kusafirisha Ng’ombe kwenye mabehewa yasiyokuwa na paa la kuzuia mvua na jua, kujaza Ng’ombe kupita kiasi na kuwabana kama mizigo, kuwanyima chakula na maji kwa siku kadhaa, kuwachapa kwa kutumia fimbo au kitu chochote kile na kuwafinya mikia.
Ni ukatili wa hali ya juu kwa Taifa lianalojigamba kuwa na amani na lenye kufuata mfumo wa demeokarsia.

Angalia tena manyanyaso mengine ya Ng’ombe kwa njia ya Barabara. Ng’ombe wanasafirishwa kutoka mikoani kwa kutumia magari ambayo kisheria hayakidhi matakawa ya kusafirisha Ng’ombe.
Wafanyabiashara wanatumia magari ya mizigo ambayo hayana paa la kuzuia mvua na jua na ili waendelee kupata faida kubwa, basi Ng’ombe watajazwa na kubananishwa kama mizigo kiasi kwamba wanakosa hata nafasi ya kugeuka au kukaa chini, kibaya zaidi ni pale wasindikizaji wanapokuwa wanawapiga sana Ng’ombe kwa kutumia fimbo, na pia ikitokea Ng’ombe atakaa chini basi huo unaweza ukawa mwisho wa maisha yake ndani ya safari kwa kukanyagwa na wenzie, hii yote inatokana na kubanana kama mizigo.

Embu angalia pale kwenye mnada wa mifugo wa Pugu unaosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, pale kuna Afisa Mifugo, Askari Polisi na pembeni kuna Kituo kidogocha Polisi, lakini hata siku moja sijasikia mtu kashitakiwa kwa kumnyanyasa Ng’ombe, je Afisa Mifugo na Askari Polisi hawafahamu kuwa kuna sheria zinazowalinda wanyama kutokupata manyanayaso yanayotendeka pale? kwani utakuta Ng’ombe wanapigwa sana hasa wakati wa kupakia na kuwashusha.
Kibaya zaidi Ng’ombe watajazwa na kulazimishwa kuingia kwenye magari hata kama nafasi hakuna, na pia ukibahatika kuwaona Ng’ombe wanaoshushwa kwenye magari au mabehewa utawaonea huruma sana kwani utawaona wengi matumbo yao yameingia ndani,yaani wananjaa ya muda mrefu, wamechoka sana na wengine wamekonda.

Na pia huwa kunakuwa na watoto wa Ng’ombe {ndama} ambao kisheria hawaruhusiwi kupelekwa pale, na ndio maana Ng’ombe wote wakifika pale ni lazima wapelekwe wakanywe maji na kula majani, na kupigwa mnada siku inayofuata.

Je serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mfugo inafanya nini katika kilinda na kutetea maslahi ya wanyama hao, au shughuli yao kubwa ni kukusanya mapato tu?
Taifa jema litaonekana jema iwapo litajali Binadamu na viumbe hai wote wakiwemo Ng’ombe.

Ukweli ni kwamba iwapo walaji wa nyama ya Ng’ombe wangeona na kutambua ni jinsi gani Ng’ombe wanavyotendewa ukatili kabla ya kuchinjwa wangeacha mara moja kula, kwani inafahamika kuwa Binadamu ameumbwa kuwa na huruma

Lengo langu siyo kuzuia biashara ya Ng’ombe ila ni kutoa dukuku langu la muda mrefu ambapo ninasosoneneka sana nikiona Ng’ombe wakiteseka ndani ya nchi yetu bila ya kuona waliyopewa jukumu la kusimamia mifugo hawashituki wala kuchukua hatua zozote kwa wanaovunja sheria za haki za wanyama nchini Tanzania

Mwisho naomba wizara ya maendeleo ya mifugo ambayo ipo chini Serikali ya Muheshimiwa Jakaya M, Kikwete yenye kauli mbiu ya Kasi Mpya, Ari Mpya, na Nguvu Mpya. Watumie kauli mbiu hii kuleta maslahi bora ya haki za wanyama kufuata Kanuni, Taratibu na Sheria za Nchi za usafirishaji wa Wanyama.

Mtetezi wa haki za wanyama
Animalactivisttz@yahoo.com
0746 027419

0 Comments:

Post a Comment

<< Home